? Baada ya mazishi ya mke wangu, moyo wangu uligeuka kuwa kivuli.
Muda wote nilikuwa kimya, hata mboni za macho zilionekana zimekufa ganzi. Mtoto wetu wa kike alinitazama kwa huzuni, lakini sikuweza kuwa baba kamili kwake. Nilihitaji kuondoka — si kwa sababu nilimchoka, bali kwa sababu nilihitaji kujiponya ili nimsimamie vyema siku moja.
Mimi, Ibrahim Khalid wa Baghdad, nilifunga safari kuelekea… nyumbani kwangu niliyoiacha miaka mingi iliyopita.
Nilirejea Baghdad nikiwa si yule kijana tajiri wa kanzu na mafuta ya miski, bali mwanamume aliyeonja utamu wa upendo, na machungu ya kuupoteza.
Nilifika wakati jua linazama — miale yake ikichora maandishi ya rangi kwenye kuta za mji. Mji wa Baghdad ulikuwa umepanuka, lakini mtaa niliokulia haukubadilika sana: ule harufu ya unga wa ngano, sauti za wauza tende, na mwangwi wa watoto wakicheka mitaani.
Niliamua kuanza polepole — siku moja nikakutana na mtu ambaye hakuwa wa kawaida.
? Mlevi Anayesema kwa Lugha ya Hekima
Alikuwa amekaa kwenye kivuli cha mtende, karibu na soko la Al-Khayrat. Mavazi yake yalikuwa yamechakaa, uso wake ulijaa mikunjo, lakini macho yake yalikuwa makini — kana kwamba yaliona zaidi ya macho ya kawaida.
Alikuwa mlevi. Lakini si mlevi wa kawaida.
Alizungumza peke yake, akicheka, kisha akamwambia paka aliyekuwa karibu:
“Hata kifaranga cha tai hufundishwa kuruka kabla ya kung’ara midomoni mwa watu.”
Nilisimama. Nikamkaribia.
Akanitazama — kisha akasema:
“Karibu, Ibrahim wa Misri.”
Nikashituka. Sikumwambia jina langu. Sikumwambia nimetokea wapi.
Nikasema kwa mshangao:
“Umenijuaje?”
Akatabasamu kwa upole, akanywa tone la divai kisha akasema:
“Mbona harufu ya maumivu haijifichi? Na macho ya mtu aliyependa hayajifichi — yanasema kwa sauti hata kimya kikilia.”
Niliketi pembeni yake. Sikuwa na haraka. Mara ya kwanza, sikuona aibu kuzungumza na mlevi hadharani. Kulikuwa na usalama fulani ndani yake, utulivu wa ajabu, na maneno ya kunitafakarisha.
? Mialiko ya Siri
Baada ya saa moja ya mazungumzo ya ajabu ajabu yaliyojaa mafumbo, akanieleza:
“Leo siyo siku ya mwisho… njoo kwangu usiku huu. Uje unisome nami nikuonyeshe waliosahau maana ya kunywa.”
Nilitabasamu, nikijua haya si mazungumzo ya kawaida.
"Upo wapi?" nikauliza.
Akanipa maelekezo ya njia ya kupinda, lango la kuteleza, nyumba yenye taa tatu zisizowaka. Akasema:
“Ukifika, usigonge mlango. Simama tu. Nitajua uko nje.”
Nilihisi kama nimealikwa kwenye fumbo. Siku hiyo usiku, nilivaa kanzu yangu nyeupe niliyorithi kwa mke wangu. Nikafika pale aliposema.
Taa hazikuwaka, lakini nilihisi macho yananitazama.
Kwa sekunde tatu…
…mlango ukafunguka wenyewe.
Ndani, kulikuwa na harufu ya udi wa India, vitabu vya kale, na vyombo vya kale vya kioo.
Lakini… siyo nyumba ya mlevi wa mtaa.
Hii ilikuwa ni nyumba ya mtu mwenye elimu, maarifa, na siri kubwa.
?️ Mwisho wa Sehemu ya 5
Katika sehemu inayofuata...
Je, kijana wetu atagundua nini katika nyumba ya ajabu ya mlevi?
Nani hasa huyu mlevi mwenye hekima nyingi kuliko wanafalsafa wa mji?
Na ni kwa nini alimvuta Ibrahim katika himaya yake?